Date: 
15-04-2024
Reading: 
Mathayo 14:13-21

Jumatatu asubuhi tarehe 15.04.2024

Mathayo 14:13-21

13 Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.

14 Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.

15 Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula.

16 Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.

17 Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.

18 Akasema, Nileteeni hapa.

19 Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano.

20 Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa.

21 Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.

Bwana huchunga na kulisha kundi lake;

Ishara hii ya kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili ni ishara inayojulikana sana. Ni ishara pekee inayopatikana katika Injili zote nne;

Mathayo 14:13-21

Marko 6:30-44

Luka 9:10-17

Yohana 6:1-4

Katika Injili zote, wanafunzi wanamwambia Yesu mwishoni, jioni baada ya huduma ya kutwa nzima aage mkutano ili watu wakajitafutie chakula. Huo mkutano haukutarajiwa wala kupangwa, ndiyo maana Yesu aliambiwa watu watawanyike. 

Yesu hakuwa tayari watu waondoke, alitaka wapate chakula. Mathayo anaandika kama tunavyoona kwenye somo letu;

Mathayo 14:16

Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.

Yohana pia anaandika vizuri kwamba Yesu alitaka watu wapewe chakula;

Yohana 6:5-6

5 Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?
6 Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda.

Yesu alitaka kuwapa watu chakula ambao wanafunzi walitaka waondoke! Yeye (Yesu) hakutaka waondoke bila kupata chakula. Hadi hapa alionesha kutaka kulisha watu wale wote. Huyu ndiye Kristo alishaye na kuchunga watu wake. Huwapokea, huwatunza na kuwaongoza wote wamwaminio na kumpa maisha yao. Tukichungwa na Yesu tunakuwa na mwisho mwema. Amina.

Tunakutakia wiki njema.

Heri Buberwa