Date: 
12-05-2025
Reading: 
2 wafalme 20:1-11

Hii ni Pasaka

Jumatatu asubuhi tarehe 12.05.2025

2 Wafalme 20:1-11

[1]Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.

[2]Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA akasema,

[3]Nakusihi, BWANA, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.

[4]Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la BWANA likamjia, kusema,

[5]Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa BWANA.

[6]Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.

[7]Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.

[8]Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba BWANA ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa BWANA.

[9]Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kwamba BWANA atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?

[10]Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.

[11]Isaya nabii akamlilia BWANA; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi.

Ndani ya Yesu kuna maisha mapya;

Somo la asubuhi ya leo linatuangazia kuugua kwa Hezekia na sala yake kwa Bwana kama tulivyosoma. Habari hii imeandikwa mara tatu katika Bibla kama ifuatavyo;

-2 Wafalme sura yote ya 20

-2 Nyakati 32:24-33

-Isaya 38 

Kuandikwa kwa habari hii mara tatu ni udhihirisho wa umuhimu wake katika kujenga Kanisa la Mungu kiimani. Habari hii ikisomwa na kufafanuliwa vizuri na kukaa mioyoni, ipo nguvu ya tofauti yaweza kutokea maishani mwetu. Kuliona hili, fuatana nami;

Mazingira ya Sala ya Hezekia;

Inakadiriwa kuwa Hezekia aliishi kati ya mwaka 739/41 hadi 686KK na aliitawala Yuda. Katika kutawala kwake, upo wakati aliugua kama tulivyosoma. 

Hezekia aliugua ugonjwa ambao alitakiwa kupokea kitu ambacho dawa ya kawaida isingeweza kutibu. Ilijulikana aliumwa majipu kwenye ngozi ya mwili wake, na kwa kukosa tiba historia yake ingebadilika. 

Hezekiah alikuwa mwaminifu kwa Mungu. Alilirejesha hekalu, akaachana na ibada za sanamu akimtumikia Mungu kwa bidii. Kuna wakati alishinda vita na kuua wapiganaji 185,000 kwa msaada wa Bwana. Lipo jambo moja hakuweza kuliondoa; alitaka kugeuza alichokifanya Baba yake, Ahazi. Ashuru walipoiharibu Israeli ya Kaskazini kama walivyoombwa na Ahazi, Israeli wengi waliingia Yuda kama wakimbizi. Hezekiah aliwasaidia kukaa Yuda akijiapiza kulipiza kisasi kwa waAshuru. 

Hezekia aliifanya Misri mshirika wake. Aliendelea kuandaa vita ingawa Nabii Isaya alitumwa kumuonya juu ya maandalizi yake ya vita. Kwa upande mmoja, Hezekia alimfanya Bwana sanamu hekaluni ambaye hakuisikia sauti yake katika nyakati muhimu kwa wakati wake japokuwa alimwabudu na kumtumikia Bwana. Ni kosa pekee Hezekia alilofanya, lakini matokeo yake yalikuwa makubwa. Uasi wake ulishindwa na watu wengi waliuawa.

 Hali ilipokuwa ngumu Hezekia alitoa dhahabu na mapambo kama malipo kwa waAshuru. Kumbukumbu za Agano la kale huonesha kuwa Hezekiah alitoa binti zake kwa waAshuru ili waondoke katika Yuda, lakini bado hawakuondoka wakitaka kupewa zaidi. Hii ilimfanya Hezekia kudhoofu, akakata tamaa na kuugua. (Paul Brown, OT)

Maelezo hayo yanatuleta kwenye somo la leo.

Somo lenyewe;

Isaya alimletea Hezekia neno la Mungu akimwambia angekufa. Ugonjwa wa Hezekia ulisababishwa na dhambi. Pamoja na Hezekia kufanya vizuri kwenye mambo mengine yote, alishindwa kwa ukaidi wake akaingia vitani na Ashuru. Hezekia alilia sana akitaka kurekebisha makosa yake lakini Mungu alikuwa mkali kwake akitaka kuuondoa uhai wake. 

Katika mstari wa tatu (soma juu kwenye somo) anaomba rehema mbele za Mungu. Katika hali ile, anaongelea ukamilifu wake machoni pa Mungu. Mungu alisikia sala yake na kupitia nabii Isaya akamwambia hangekufa, bali angemwongezea miaka kumi na mitano. 

Kupitia habari hii ya Hezekia, yapo mambo kadhaa kuhusu Mungu wetu alivyo;

-Mungu huona machozi ya wamliliao;

Machozi ya Hezekia hayakuwa ya kawaida. Kumbuka alipoteza watu wengi wa nyumbani mwake kwa kuingia vitani, aliwatoa binti zake kuwalinda watu wake. Aliwaweka watu wake mbele kuliko familia yake. Ni ngumu kulinganisha, kama ambavyo ingekuwa inafikirika Mungu alijisikiaje kumtoa mwanae wa pekee kuokoa wenye dhambi

-Mungu alitoa miaka kumi na mitano kwa masalia katika Yuda na ufalme kwa ujumla. Ilikuwa nafasi kwa Israeli kurudi katika hali yake. 

-Miaka kumi na mitano pia ilimhusu Hezekia. Alipewa ili kurekebisha makosa yake.

Somo tulilosoma linaeleza wazi kuwa ilikuwa vigumu kwa Hezekia kuamini kwa yeye na Yerusalemu wangerudi katika hali ya kawaida. Alitaka ishara.;

2 Wafalme 20:8-11

[8]Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba BWANA ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa BWANA.
[9]Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kwamba BWANA atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?
[10]Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.
[11]Isaya nabii akamlilia BWANA; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi.

Tafsiri ya ishara hapo juu ni kuwa Hezekia aliomba kurudishwa kwa Taifa kabla hajakosa. Isaya alijibu kwamba Mungu angerejeza kivuli hatua kumi nyuma, yaani kurejesha hali ya awali.

Hitimisho;

Baadhi yetu kuna wakati tunaishi isivyompendeza Mungu kwa sababu ya kutoisikia sauti yake. Tusipokutana na magumu huko, inakuwa vigumu kusikia maonyo ya Bwana. 

Nitumie mstari maarufu;

Yohana 3:16

[16]Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Neno "asipotee" ni maarufu sana lakini ukweli ni kuwa kuna wakati ni vigumu kulisikia na kulifanyia kazi. Unaweza kuwa umechelewa kutambua kuwa "umepotea", sasa huo siyo wakati wa kutafuta sababu na kutokubali kukosa. Neno la leo linatuelekeza "Sala ya imani" na siyo maonesho. Tukitubu Mungu anatuondolea kukata tamaa na kutuponya kama ilivyotokea kwa Hezekia.

Hezekia aliona ishara na matibabu yake yakawa rahisi. Mkate wa tini uliwekwa kwenye jipu akapona. Wakati huohuo waashuru 185,000 waliangamia nje ya Yerusalemu kwa tauni. Hezekia ni shujaa wa katika somo la leo, ambaye pamoja na yote aliyopitia bado aliponywa kwa Imani. Tumfuate Kristo kwa kuisikia sauti yake, naye hutupa haja zetu kwa Imani. Tutafakari juu ya maisha yetu kama kweli tunayo Imani katika Kristo. Kumbuka Imani bila matendo imekufa kama Yakobo alivyoandika;

Yakobo 2:26

[26]Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa. Amina

Uwe na wiki njema

 

Heri Buberwa Nteboya