Date: 
27-06-2022
Reading: 
Yeremia 35:12-19

Jumatatu asubuhi tarehe 27.06.2022

Yeremia 35:12-19

12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,

13 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema Bwana.

14 Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi.

15 Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza.

16 Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi;

17 kwa sababu hiyo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize; nimewaita, wala hawakuniitikia.

18 Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote, na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru;

19 basi, kwa sababu hiyo, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.

Wito wa kuingia ufalme wa Mungu;

Leo asubuhi tunamsoma Nabii Yeremia akitumwa kupeleka ujumbe kwa Taifa la Mungu, kwamba kwa nini hawakusikia na kulitii neno lake. Mungu alituma wajumbe wake, sasa anahoji kwa nini hawakusikilizwa? (14). Kwa kutomsikiliza, Mungu anawapa ujumbe wa kuleta mabaya juu yao (17). Yeremia aliupeleka ujumbe huu, akiwaambia watu kufuata neno la Mungu kama walivyoamriwa.

Sauti ya Mungu inatujia wiki hii ikitutaka kumsikiliza yeye. Anatujia kwa njia ya neno lake kupitia kwa watumishi wake. Tujihoji kila mmoja kwa nafasi yake; Tunamsikiliza Mungu na kumfuata? Huu ni wito tunapewa na Bwana, yaani kumsikia na kumfuata. Tusipoitika hatuwezi kuingia kwenye ufalme wake.

Tunakutakia wiki njema iliyojaa neema katika ufalme wa Mungu.

 

Heri Buberwa

Mlutheri