Date: 
24-02-2023
Reading: 
Mathayo 6:16-18

Hii ni Kwaresma 
Ijumaa asubuhi tarehe 24.02.2023

Mathayo 6:16-18
16 Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Tunaitwa kuishi maisha ya toba;

Asubuhi hii tunasoma sehemu ya mafundisho ya Yesu pale mlimani. Sehemu hii huitwa hotuba ya mlimani, ambapo Yesu alifundisha yapasayo juu ya ufalme wa Mungu. Tunaona Yesu akifundisha juu ya kutojionesha wakati wa kufunga, bali kufunga iwe ni katika Bwana.

Kujionesha mbele za watu kama mwenye haki ni tatizo siku hizi. Zaidi ya hapo, baadhi yetu tunajiona bora katika ufalme wa Mungu kuliko wengine. Tunafikiri tukionekana tunasali, tunafunga, tunatoa sana, tunaimba, tunahubiri n.k ndipo tuko na Bwana! Tuutafute uso wa Mungu na siyo kujionesha, ndipo tutaurithi uzima wa milele.
Siku njema.

Heri Buberwa