Date: 
24-11-2023
Reading: 
2Wathesalonike 2:6-12

Ijumaa asubuhi tarehe 24.11.2023

2 Wathesalonike 2:6-12

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;

10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.

Hukumu ya mwisho inakuja;

Mtume Paulo anawaandikia Wathesalonike juu ya ujio wa Kristo, kwamba wanao muda ambao Kristo hajaja ili waamini. Anawasihi kuamini, maana wasioamini watahukumiwa kwa kutokuamini kwao. Paulo anasisitiza kutoamini mafundisho ya uongo, maana hata hao wafundishao uongo watahukumiwa pia. Msisitizo wa Paulo ni Injili sahihi ya Yesu Kristo.

Tunaweza kumrejea Paulo hata sasa kwa somo hili, kwamba mafundisho ya uongo yapo sana siku hizi.

Kama Paulo alivyosema, sisi kama waaminio tusiyaamini. Hatutayaamini mafundisho ya uongo kwa msaada wa Yesu Kristo aliyetuita. Kama vile imani yetu ilivyo katika Kristo, tuzidi kudumu katika yeye, ili tuurithi uzima wa milele. Amina.

Ijumaa njema.

 

Heri Buberwa