Date: 
02-12-2023
Reading: 
Luka 19:11-27

Jumamosi asubuhi tarehe 02.12.2023

Luka 19:11-27

11 Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara.

12 Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.

14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23 basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.

27 Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.

Maandalizi kwa uzima wa milele;

Yesu anatoa mfano wa kabaila mmoja aliyesafiri kwenda nchi ya mbali. Aliwapa watumwa wake mafungu ya fedha. Mmoja alizalisha mafungu kumi mengine toka kwenye mafungu kumi, akawekwa juu ya miji kumi. Mwingine alichukua mafungu matano akazalisha mengine matano, akawekwa juu ya miji mitano. Kuna ambaye hakuzalisha hata fungu moja, akanyang'anywa hilo fungu moja!

Tunaona kila mmoja akilipwa kulingana na alichozalisha. Hapa linakuja wazo la kila mmoja kuhukumiwa kwa kadri ya matendo yake kama Mtume Paulo anavyoandika;

Warumi 2:5-6

5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,
6 atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;

Yohana pia alifunuliwa;

Ufunuo wa Yohana 20:13

Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

Kumbe tutahukumiwa kwa kadri ya matendo yetu. Hivyo imani yetu iwe thabiti ili tutende mema, tayari kuurithi uzima wa milele. Amina.

Jumamosi njema.

Heri Buberwa