Date: 
16-12-2023
Reading: 
2 Wakorintho 10:12-18

Jumamosi asubuhi tarehe 16.12.2023

2 Wakorintho 10:12-18

12 Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili.

13 Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu.

14 Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo;

15 wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada;

16 hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.

17 Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana.

18 Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.

Yesu anakuja katika Utukufu wake;

Mtume Paulo analiandikia Kanisa la Korintho juu ya waamini wanaojisifu. Anasema hakuna haja ya kujihesahu pamoja na wanaojisifu wala kujilinganisha nao maana hawana akili. Paulo anakazia Injili ya Kristo kuwa mwongozo kwaa kila aaminiye, na siyo kujisifu. Kwa mujibu wa Paulo, maisha ya aaminiye lazima yawe ya kulishika neno la Mungu na kutenda yapasayo.

Mtume Paulo anamalizia kwa kusema kuwa yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana, maana mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.

Mtume Paulo anatukumbusha kutenda mambo yote katika Bwana, tukimpa yeye Utukufu daima ili tuwe na mwisho mwema. Amina.

Jumamosi njema.

 

Heri Buberwa