Date: 
28-03-2024
Reading: 
Mathayo 26:26-29

Hii ni Alhamisi Kuu tarehe 28.03.2024

Masomo;

Zab 4:1-8

1Kor 10:14-16

*Mt 26:26-29

Mathayo 26:26-29

26 Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu

27 Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;

28 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

29 Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.

Agano jipya kwa damu ya Yesu;

Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakisherehekea Pasaka ile ya siku zote aliposema maneno tuliyayosoma hapo juu. Walikuwa wakisherehekea jinsi walivyokombolewa kutoka utumwani. Lakini wakiendelea kusherehekea, ndipo Yesu anatwaa mkate na kuumega, akiwaambia huu ndio mwili wangu, twaeni mle kwa ukumbusho wangu. Na divai vivyo hivyo.

Hadi hapo sherehe hiyo haikuwa tena ya kuadhimisha ukombozi toka Misri. Yesu alikuwa akitambulisha Agano jipya kwa ondoleo la dhambi, yaani mwili na damu yake. Alikuwa anajitangaza kuwa yeye ndiye mwanakondoo wa Pasaka. Ukombozi haukuwa tena kwa damu ya mwanakondoo, kama Pasaka ya zamani, bali ukombozi sasa ulikuwa kwa damu ya Yesu. 

Kwa nini ilibidi kutokea hivi?

Katika Agano la kale, walitoa sadaka ya mwanakondoo na sadaka nyinginezo ili kusamehewa dhambi. Lakini baadae kwenye Agano imeandikwa;

Waebrania 10:4

[4]Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

Zile sadaka hazikusamehe dhambi kamwe, zilikuwa ni picha tu, na alama ya sadaka ya ondoleo la dhambi kupitia Mesiya ajaye, Yesu Kristo.

Karamu ya Yesu inatuonesha Yesu alivyojitoa sadaka kwa ajili yetu. Yesu alisema mkate ni mwili wake na mvinyo ni damu yake kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Ni muhimu kuelewa kuwa hizi ni alama zisizo na "nguvu ya kuokoa" ndani yake. Kula mkate na kunywa mvinyo hakuondoi dhambi zako. Mtume Paulo anaeleza vizuri;

1 Wakorintho 11:24-25

[24]naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
[25]Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

Yesu alisema "....kwa ukumbusho wangu". Ni alama. Tunakumbuka gharama aliyotoa kwa dhambi zetu. Mwili wa Yesu uliwambwa msalabani, damu yake ilimwagika.

Sasa basi;

Hatuwezi kufanya ukumbusho wa Yesu kutuokoa kwa kufanya yasiyofaa. Hivyo ni muhimu kujichunguza kwanza kabla ya kujongea Altareni kushiriki mwili na damu takatifu. Hatuwezi kukumbuka ukombozi wetu tukiwa waongo, wezi, wasengenyaji, vibaka, waonevu, wanafiki, wazinzi, mafisadi n.k Hivyo kukumbuka ukombozi wetu ni tangazo la kutubu na kurejea kwa Bwana. Ndio maana kwa pale Kanisa linapoona mtu hajaenenda sawa, anakuwa chini ya marudi. (Low church huita nje ya kundi), pia mtu hushauriwa kuishi maisha ya toba na msamaha ili kushiriki kwa ukamilifu wake. Leo tunashiriki Meza takatifu. Nini nafasi yako? Maisha yako yanaakisi ushiriki wako mezani ukikumbuka kukombolewa kwako?

Nilitaka ujue kuwa, tunapokumbuka wokovu wetu kwa njia ya mwili na damu ya Yesu, tunawajibika kuishi maisha ya uchaji, tukiwa watu wa toba na msamaha. Tunafanya kwa ukumbusho wake tukiwa wenye mioyo safi.

Ujumbe mkuu;

Jumapili iliyopita tuliona Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe. Tuliona akijitambulisha kama Mesiya na mfalme. Pia alijitambulisha kama mwanakondoo wa Pasaka.

Tumeona hapo awali kuwa Israeli walisherehekea Pasaka kwa kuchinja mwanakondoo wakikumbuka jinsi walivyokombolewa toka utumwani Misri.

Sasa leo, Yesu anapotoa mwili na damu yake, akituasa kula na kunywa kwa ukumbusho wake, anatukumbusha kuwa yeye ndiye mwanakondoo wa Pasaka. Yeye ndiye aliyemwaga damu yake kwa ajili ya dhambi zetu. Hatuchinji tena kondoo, bali tumeokolewa kwa damu ya Yesu Kristo.

Hivyo basi;

1. Tukumbuke kuwa mwili na damu ya Yesu ni kwa ajili ya kusafisha dhambi zetu.

2. Yesu ndiye mwanakondoo wa Pasaka, hivyo Yesu ndiye Mwokozi.

3. Tuiendee karamu ya Bwana kwa usafi wa mioyo yetu. Hatuwezi kumkumbuka Yesu tukiwa waovu.

Hii ni Alhamisi Kuu

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com