Date: 
01-07-2025
Reading: 
Mathayo 5:27-32

Jumanne asubuhi tarehe 01.07.2025

Mathayo 5:27-32

27 Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

29 Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

30 Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

31 Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;

32 lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

Wito wa kuingia Ufalme wa Mungu;

Yesu anahutubia mlimani, na katika sehemu tunayosoma leo anaanza kwa kurejea Agano la kale, ambapo ilikuwa marufuku kuzini. Adhabu ya kuzini ilikuwa kali sana, mfano tunaupata pale Mafarisayo na waandishi walipompeleka mwanamke mzinzi mbele ya Yesu;

Yohana 8:4-5

4 Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.
5 Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

Yaani yule mwanamke alitakiwa kupigwa mawe! Lakini Yesu anakazia zaidi, kwamba kila amtamaniye mwanamke amekwisha kuzini naye moyoni mwake! Yesu anazidi kufundisha kuwa jicho la kuume likikukosesha ling'oe ulitupe mbali, na mkono vile ile, ili kiungo cha mwili wako kisisababishe uende jehanamu. Yesu alikuwa anafundisha juu ya kumuishia yeye ili kuingia katika Ufalme wake. Tumuishie Kristo ili tuurithi uzima wa milele. Amina

Siku njema

Heri Buberwa