Date: 
08-08-2025
Reading: 
1Wafalme 4:29-34

Ijumaa asubuhi tarehe 08.08.2025

1 Wafalme 4:29-34

29 Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.

30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.

31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.

32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.

33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.

Tunaitwa kuzaa matunda mema;

Suleimani alimpenda sana Bwana, akienda katika amri za Babaye. Alidumu katika kufukiza uvumba hekaluni. Bwana akamtokea na kumwambia aombe lolote. Suleimani akasema kwa kuwa alikuwa ametawazwa kuwa Mfalme, basi Bwana amjalie hekima ili aweze kuwaongoza watu wa Mungu kwa haki. Basi Mungu akamjalia hekima, akaongoza kwa moyo wa hekima akitoa hukumu za haki. Kesi maarufu zaidi ni ya wanawake wawili waliokwenda kwake wakigombania mtoto, baada ya mmoja kufiwa na mwanae. Suleimani aliamuru yule mtoto mzima akatwe katikati, mama halali akalia mbele za Mfalme, ikaamuriwa apewe mtoto wake!

Sasa ndipo somo linasema Suleimani alipewa hekima na akili nyingi sana na moyo mkuu kama mchanga wa Pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima zote kwa wakati ule. Watu walisafiri umbali mrefu kwenda kuisikia hekima ya Suleimani. Tunachoona kwenye somo ni kuwa Suleimani alijitoa kumtumikia Bwana, akaomba hekima, na katika utume wake alimzalia Bwana matunda maana aliomba hekima ambayo aliitumia kuwaongoza watu wa Mungu kwa hekima na hukumu za haki. Tutumie nafasi zetu kumzalia Mungu matunda. Amina

Nanenane njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com