Jumanne asubuhi tarehe 12.08.2025
1 Samweli 12:12-15
12 Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa Bwana, Mungu wenu, ni mfalme wenu.
13 Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, Bwana ameweka mfalme juu yenu.
14 Kama mkimcha Bwana, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya Bwana, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata Bwana, Mungu wenu, vema!
15 Bali msipoisikia sauti ya Bwana, mkiiasi amri ya Bwana, ndipo mkono wa Bwana utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu.
Uchaguzi wa busara;
Leo asubuhi tunasoma sehemu ya hotuba ya Samweli akiwa mzee kwa Israeli, hotuba ambayo inaaminika ilikuwa ni ya kuwaaga wana wa Israeli. Ukisoma kuanzia sura ya 12 mwanzoni, unaona Samweli akirejea historia ya kukombolewa kwa Israeli, akisimulia walivyokombolewa kutoka utumwani. Anawataka Israeli kuona jinsi Mungu alivyowatendea matendo makuu. Katika somo Samweli anawaasa kumcha Bwana na kumtumikia, na kamwe wasimuasi Bwana wao ili mkono wa Bwana uwe juu yao.
Angalia mkazo wa Samweli kwa Israeli;
1 Samweli 12:24-25
24 Mcheni Bwana tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu. 25 Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.Samweli anawaita Israeli kumtumikia Bwana kwa mioyo yao yote, wakikumbuka matendo yake makuu. Anakazia kuwa wakiendelea kutenda mabaya wataangamia. Tunakumbushwa kuchagua kudumu katika Imani kama tulivyompokea Kristo, ili atupe uzima wa milele. Kinyume chake tutaangamia. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650