Event Date: 
25-10-2020

KKKT Azaniafront yaadhimisha ‘Sikukuu ya Mavuno’ kwa mwaka 2020

Siku ya Jumapili, tarehe 25/10/2020, Usharika wa KKKT Kanisa Kuu la Azaniafront ulifanya maadhimisho ya sikukuu ya mavuno, sikukuu ambayo hufanyika kila mwaka kwa washarika kumtolea Mungu sehemu ya matunda ya kazi wanazozifanya.

Ibada ya kusherehekea sikukuu hii ya mavuno kwa mwaka 2020 ilifanyika katika viwanja vya usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront huku ikihudhuiriwa na washarika waliojitokeza kwa wingi wakiwa na mavuno yao tayari kwa kumtolea Mungu.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, akisaidiana na Mch. Mwaipopo na Mch. Mlaki. Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, aliwapongeza washarika wa Azaniafront kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria ibada hiyo huku akisisitiza umuhimu wa sikukuu ya mavuno katika maisha ya kikristo.

“Leo ni siku ya ushuhuda juu ya namna ambavyo Mungu ametubariki katika mwaka huu wa 2020. Mavuno haya mliyoleta leo ni kwa ajili ya kusaidia kazi ya kuhubiri injili,” alisema Baba Askofu.

Baba Askofu Dk. Alex Malasusa akiwa na baadhi ya wazee wa kanisa wakati wa ibada ya Mavuno iliyofanyika usharikani.

Baba Askofu aliongeza kuwa, watu wote bila kujali umri, jinsia wala hali ya uchumi wanapaswa kumshukuru na kumtanguliza Mungu katika shughuli zao zote wanazozifanya.

 Baadhi ya washarika waliohudhuria ibada ya mavuno wakifuatilia kwa makini 

Kwaya ya AIC, Chang'ombe ikiimba katika kilele cha sikukuu ya mavuno katika usharika wa Azaniafront

Wazee wa kanisa wakiwa wamejipanga tayari kwa ajili ya kupokea mavuno kutoka kwa washarika wa Kanisa Kuu Azaniafront

Baadhi ya mavuno yaliyowasilishwa na washarika

Aidha, Baba Akofu Malasusa aliwakumbusha washarika juu ya umuhimu wao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika nchini Tanzania mnamo tarehe 28/10/2020.

Ibada ya sikukuu ya mavuno katika Usharika wa Azaniafront ilienda sambamba na ibada nyingine za aina hiyo zilizofanyika katika sharika zote za Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Picha zaidi, tembeleahttps://photos.app.goo.gl/WGedvUY5XB9QMedB6